LENGO mojawapo la Elimu ya Msingi Tanzania ni kumuandaa mtoto aweze
kuingia hatua ya pili ya elimu yaani Sekondari na Elimu ya Ufundi lakini
pia kumwandaa mtoto kuingia katika ulimwengu wa kazi na ajira.
Nikitafakari kwa makini naona ni wazi kuwa lengo hili halifikiwi kwani
watoto wengi wanaomaliza elimu ya msingi hawapati nafasi ya kuendelea
na masomo ya sekondari au mafunzo ya ufundi na badala yake hurudi
kijijini/mitaani na kuwa wanakijiji/wa mtaani.
Baadhi ya watoto hawa huwa hawajui kusoma na kuandika kutokana na hali
halisi ya mfumo wa elimu ya Tanzania ulivyokaa na hawapati elimu
ya uraia itakayowasaidia endapo hawataendelea na masomo. Elimu waipatayo
inawaandaa kufaulu mtihani ili kuendelea na masomo na huwapa mwanga
kidogo sana wa kuzikabili changamoto za maisha wale ambao hawapati
fursa ya kuendelea na masomo.
Watoto hawa wanaofeli mtihani bado ni wadogo na mfumo wa elimu ya
msingi hauwaruhusu tena kurudi shuleni ili kurudia masomo yao, Wengi wa
watoto hawa hutoka familia maskini zenye vipato vya chini hivyo
huwawia vigumu kujiunga shule za binafsi na kama ikitokea ni kwa
wachache ambao wazazi wao ama ni watumishi ama wafanya biashara wenye
kipato kinachoeleweka.
Kama nilivyosema hapo mwanzo, watoto hawa hupata elimu inayowaandaa
kufaulu mtihani wa mwisho wa Darasa la Saba ili kuendelea na masomo ya
sekondari kwahiyo watakao faulu, elimu itakuwa imewanufaisha lakini wale
wasiobahatika elimu inakuwa haijawasaidia na watarudi nyumbani kuishi
na wazazi wao katika hali zao za umaskini.
Kumbuka kuwa hakuna elimu ya ujasiliamali inayofundishwa ili kuwandaa
watoto hawa kuwa wajasiriamali, au elimu ya uraia itakayowaandaa
kukabiliana na changamoto za maisha pindi warudipo nyumbani, wala hakuna
chochote wanachokuwa wameandaliwa watakapofeli mtihani kwamba wanaweza
kukifanya ili kujimudu kimaisha, wanakuwa hawana mtaji wa namna yoyote
ile; si maarifa wala fedha.
Watoto hawa hupelekwa shuleni kutimiza wajibu kwa vile elimu ya msingi
ni ya lazima kwa kila mtoto lakini hakuna anachoenda kukivuna zaidi ya
kufikiria kufaulu mtihani kwenda sekondari na hali hii huendelea
kuchangia umaskini kwa kiasi kikubwa nchini mwetu.
Watoto hawa hupatwa na madhara makubwa sana wasiostahili
kuyapata, madhara yanayopelekea kujiingiza katika mitandao ya ajabu na
michafu isiyofaa na kukubalika katika jamii zao ikiwemo utumiaji wa
madawa ya kulevya, ulevi wakupindukia na uvutaji sigara,
umalaya/ubakaji/ushoga/ukahaba, wizi/ukabaji/ujangili na matendo
mengine kama hayo yanayosababisha mifarakano kwenye familia na jamii kwa
ujumla.
Hali hii hutokea pale wazazi wanapoona kuendelea kuishi na watoto hao
ni mzigo na hawawezi kuwahudumia hivyo watoto kukosa mahitaji yao ya
msingi kutoka kwa wazazi wao. Hapo ndipo watoto hujiingiza katika ajira
zisizo rasmi pia ndoa za utotoni zinazo sababisha mimba za utotoni na
kupelekea zaidi umaskini na ongezeko la magonjwa ya zinaa ikiwemo
VVU/UKIMWI.
Watoto wengine huamua kujishughulisha na shughuli zingine za kiuchumi
kama vile ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kupata kuni ili
kuuza, uvuvi haramu wa kutumia sumu na zana zisizokubalika ili kujipatia
kipato kwa haraka, uwindaji haramu wa wanyama pori mambo ambayo kwa
pamoja huchangia uharibifu wa mazingira na ujangili.
Wengine hujishughulisha na utengenezaji wa pombe haramu aina ya gongo
na uuzaji wa madawa ya kulevya vinavyosababisha wao wenyewe kuwa
watumiaji na waathirika wakubwa. Watoto wengine huamua kuwa ombaomba na
kuishia mitaani na kusababisha ongezeko la watoto wa mitaani.
Kwa changamoto hizi ni vigumu kwa Tanzania kuondokana na umaskini kama
elimu ya msingi haitatazamwa na kufanyiwa marekebisho upya. Ikumbukwe
kuwa umri wa watoto hawa ni mdogo ambao ni kati ya miaka kumi na mbili
na kumi na nne na hutambuliwa na sheria kuwa ni watoto lakini
wanapohitimu na kutochaguliwa kuendelea na masomo husahaulika na kuachwa
bila msaada wowote kutoka kwa wadau wa elimu na Serikali kwa ujumla.
Hapo ndipo huamua kutafuta ajira na mara nyingi hujikuta wamejiingiza
kwenye ajira hatarishi kwao kama vile kazi ngumu za mashambani,
viwandani, migodini, na majumbani. Wakati mwingine sheria huwabana
waajiri wa watoto hawa kuwa umri wao hauruhusu kutumikishwa na hapo
ndipo najiuliza maswali haya: je, watoto hawa watajikimu vipi ili hali
hawana namna nyingine ya kutafuta kipato?
Kwa utaratibu huu tunawezaje kupunguza tatizo la watoto wa mitaani?
Tatizo la mimba za utotoni litadhibitiwa vipi?, na tutawezaje kupunguza
swala zima la ukabaji na wizi unaopelekea watoto hawa kubandikwa majina
mabaya ya vibaka na kuuwawa kikatili na pengine kwa kuchomwa moto?
Serikali na wadau wengine wote wa elimu wasipoliangalia swala hili kwa
makini na kulitafutia ufumbuzi, itakuwa ni vigumu sana kuondokana na
umaskini na kuufuta ujinga utakaotokana na kushindwa kwa watoto hawa
wanaogeuka kuwa wazazi wa umri mdogo kuwahudumia na kuwapa haki za
msingi watoto wao wanaowazaa kama vile elimu, chakula, mavazi, malazi,
huduma za afya n.k kutokana na kuwa na hali duni ya maisha wao na
familia zao na hali hii itakuwa inajirudia mwaka hadi mwaka.
Ushauri wangu kwa Serikali na wadau wote wa elimu yakiwemo mashirika
yanayojishughulisha na watoto wautazame upya mfumo huu wa elimu ya
msingi ili ama watoto hawa wapewe fursa nyingine ya kurudi shuleni
kusoma au waangalie uwezekano wa kutoa elimu maalumu kwa hawa watoto
itakayowawezesha kujiandaa kukabiliana na changamoto wanazoenda kukutana
nazo pindi warudipo uraiani.
Hii itawasaidia kupata fursa ya kujitegemea kiuchumi na kuondokana na
utegemezi na umaskini ambao naamini chimbuko lake lipo hapa, hali
itakayopelekea kukubalika katika familia zao na jamii kwa ujumla.
Sheria ya mtoto iliyowekwa iwabane wadau na Serikali kwa kuwatelekeza
watoto hawa ambao umri wao ni chini ya miaka kumi na nane na kupambana
na changamoto ambazo bado ni adhabu isiyowastahili kuipata na ninaamini
ni haki ya msingi ya mtoto huyu wa maskini kuendelea kupata elimu hadi
hapo atakapofikia umri wa utu uzima.

No comments:
Post a Comment