MGOMBEA ubunge jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Saed Kubenea ameahidi ajira za vijana wa jimbo iwapo
atachaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 25.
Amesema ajira 100,000 zitapatikana kupitia Mfuko wa Jimbo kwa lengo la kuwasaidia vijana kujitegemea.
“Ninataka kuwa mbunge kwa sababu ninajua kuna vijana wengi hawana ajira.
Tunataka kutengeneza ajira laki moja ndani ya miaka mitano. Nina
uhakika uwezo tunao,” amesema.
“Tutaweka mfumo rasmi wa ajira kupitia mfuko wa mbunge. Dhamira tunayo,
uwezo tunao na wito wa Mwenyezi Mungu tunao… wapo vijana waliomaliza
vyuo vikuu tutawatafutia ajira serikalini, kwenye mashirika ya umma na
asasi za kiraia.
“Wapo vijana wamepata elimu ya kati nao watapata ajira… ambao hawakusoma
kabisa, watakuwa na kazi hata ya kuzoa takataka katika mitaa yetu.
Ajira zipo tatizo lililopo watu waliopo serikalini wamechoka
kuwafikiria, wanajifikiria wenyewe,” amesema Kubenea.
Kubenea anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), amesema
anafurahia ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA – Chadema, Chama cha
Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
“Kupitia umoja huu, tutatengeneza taifa ambalo mtoto wa masikini anakuwa
kiongozi kwa kuwa imeshindikana kufanyika ndani ya mfumo wa CCM,”
amesema.
Amesema ameamua kugombea ubunge ili kupata fursa ya kuwanyoosha viongozi
mafisadi kwa sababu kwa kubakia kazi ya uandishi wa habari lipo suala
la sheria kandamizi zinamnyima uhuru wa kuandika maovu yanayofanywa na
viongozi wa serikali.
Aliitaja Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, Sheria ya Magereza ya mwaka 1974, Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1968 na Sheria ya Polisi, “zote zinazuia haki ya wananchi kutoa na kupata taarifa kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kutoa haki kwa kila raia kutoa na kupata habari.
“Serikali ilifungia gazeti langu la MwanaHALISImwaka
2012. Nimeenda mahakamani nimeshinda kesi. Na Jumatatu litaingia
mtaani. Kitu kinachosikitisha serikali italazimika kunilipa fidia ya
zaidi ya Sh. 6 bilioni.”
“Fedha hizi ni za walipa kodi ambazo zingetumika kusomeshea watoto wetu
na kusaidia huduma ya afya, lakini kwa uzembe na ubinafsi wa wateule wa
Rais Kikwete, mahakama imesema nilipwe fidia ninayostahili,” amesema
Kubenea.
Baada ya Waziri wa Habari, Dk. Fennela Mkangara kufungia gazeti hilo
Julai 30, 2012, mahakama imemuona waziri huyo alikosea kisheria na
kuamua serikali iachie gazeti lichapishwe bila ya kuingiliwa kwa namna
yoyote ile na serikali

No comments:
Post a Comment