Monday, November 24, 2014
MAHAKAMA KUU YAANZA KUSIKILIZA MAOMBI YA KIONGOZI JUMUIYA YA UAMSHO
MAHAKAMA KUU YAANZA KUSIKILIZA MAOMBI YA KIONGOZI WA UAMSHO.
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeanza kusikiliza maombi ya Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) na wenzake ya kuiomba mahakama ipitie kesi ya awali inayowakabili.
Kusikilizwa kwa maombi hayo, kunatokana na mashtaka ya awali ya kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi pamoja na kusaidia kufanyika kwa vitendo hivyo.
Maombi hayo yalisikilizwa jana, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Dk. Fauzi Twaib, Wakili wa Serikali Peter Njike akisaidiana na George Barasa.
Awali wakili wa utetezi, Abubakar Salum alidai kwamba wanaiomba Mahakama itoe tafsiri, kwanini watu wawili walioingizwa nchini kufanya vitendo hivyo, hawafikishi mahakamani, pia ni rai wa nchi gani.Pili mashitaka hayaonyeshi lini na eneo gani vitendo hivyo vimefanyika.
Kwa upande wake Wakili wa serikali Njike, aliiomba mahakama impe nafasi ya kusikilizwa, kwa kuwa upande wa Jamhuri ulikosa majibu kutokana na maombi hayo kufikishwa kwa hati ya dharura.
Baada ya kupewa nafasi ya kusikilizwa, Njike aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ili apate muda wa kutoa majibu kuhusu maombi hayo, Jaji Twaib aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 4, mwaka huu ili upande wa Jamhuri uweze kutoa majibu.
Hata hivyo, Jaji Twaib alisema kama upande wa Jamhuri utakuwa na jambo la ziada kuhusu maombi hayo wanatakiwa kulifikisha Novemba 28, mwaka huu.Pia kwa upande wa utetezi kama wana jambo la ziada walifikishe Desemba 1, mwaka huu.
Mbali na Farid, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala, Said Kassim, Hamis Amour, Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe.
inadaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka huu washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Wakati huo huo kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake imeshindwa kuendelea kusikilizwa kwa sababu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja ni mgonjwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment